Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia, Jackson Katabi (30), mkazi wa Kaporo, Wilaya ya Kilombero, kwa tuhuma za kumuua,George Magnus kufuatia ugomvi ulioibuka kutokana na deni la Sh1,000.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Alex Mkama, akizungumza leo, Jumatano, Aprili 2, 2025, tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 28, mwaka huu, katika kijiji cha Kaporo, Wilaya ya Kilombero huku chanzo kikiwa ni marehemu George kukaidi kulipa deni la Sh1,000 kwa mtuhumiwa Jackson Katabi.
“Katika ugomvi huo, marehemu alikumbwa na jeraha dogo kichwani, ambapo alikimbizwa katika Zahanati ya Kaporo Health Service kwa huduma ya kwanza. Baada ya kupatiwa matibabu, aliruhusiwa kurejea nyumbani, lakini akiwa njiani, alianguka na kupoteza maisha,” amesema Kamanda Mkama.
Ameongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kwamba mtuhumiwa Jackson Katabi atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.