Rais Mkongwe wa Cameroon Atangaza Nia ya Kungombea Urais Mara ya 8.

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

14 hours ago
rickmedia: rais-mkongwe-cameroon-atangaza-nia-kungombea-urais-mara-37-rickmedia

Rais wa Cameroon, Paul Biya, ambaye ndiye kiongozi mkuu mwenye umri mkubwa zaidi akiwa na miaka 92, ametangaza nia yake ya kugombea tena urais.

Mnamo mwaka 2008, Biya alifuta ukomo wa mihula ya urais, jambo lililomruhusu kugombea nafasi hiyo bila kikomo.

Mpango wake wa kugombea urais kwa mara ya nane umetangazwa jana Julai 13, kupitia chapisho kwenye akaunti rasmi ya Rais kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).

Ujumbe huo unasomeka..

“Mimi ni mgombea katika uchaguzi wa urais. Muwe na hakika kuwa dhamira yangu ya kuwahudumia inalingana na uharaka wa changamoto tunazokabiliana nazo.”

Biya, ambaye anataka kupata muhula mpya ambao unaweza kumuweka madarakani hadi atakapokaribia miaka 100, alichukua uongozi mwaka 1982 baada ya mtangulizi wake, Ahmadou Ahidjo, kujiuzulu.

Afya yake imekuwa ikitiliwa shaka mara kwa mara, hasa mwaka jana alipotoweka machoni mwa umma kwa siku 42 mfululizo.

Ingawa wengi walikuwa wanatarajia kuwa angegombea tena, haikuwa imethibitishwa rasmi hadi tangazo la Jumapili kupitia mitandao ya kijamii.

Biya amekuwa akichapisha mara kwa mara kwenye akaunti yake ya X katika siku za hivi karibuni kuelekea tangazo hilo.

Tangazo la Jumapili linatarajiwa kufufua mjadala kuhusu uwezo wa Biya kuendelea na majukumu ya urais, kwani mara chache hujitokeza hadharani na mara nyingi hukabidhi majukumu kwa mkuu mwenye ushawishi wa ofisi ya rais.

Oktoba mwaka jana, alirejea nchini Cameroon baada ya kutoweka kwa siku 42, hali iliyozua uvumi kuwa alikuwa mgonjwa. Serikali ilidai kuwa alikuwa na afya njema lakini ikakataza mijadala kuhusu hilo.