Rais wa Marekani, #DonaldTrump, amesema anataka kupata madini adimu na madini muhimu kutoka Ukraine kama sehemu ya makubaliano kwa mabilioni ya dola za msaada wa kijeshi ambao Washington imekuwa ikitoa kwa Kyiv.
Ni wazo ambalo hapo awali lilipendekezwa na Rais wa Ukraine, #VolodymyrZelenskyy, ambaye alitaka kumvutia Trump kwa mtazamo wake wa mfanyabiashara ili kuhakikisha msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Kyiv unaendelea.
Mbali na kuwa msambazaji mkubwa wa ngano, nafaka, na unga, Ukraine pia ina akiba kubwa ya madini adimu na madini muhimu.
Madini kama vile lithiamu, gallium, na neodymium ni muhimu katika utengenezaji wa teknolojia mbalimbali, ikiwemo betri za magari ya umeme na vifaa vya kijeshi vya kisasa. Kwa hivyo, Marekani na China, miongoni mwa mataifa mengine, yamekuwa yakivitamani sana.
Kauli za Trump zilitolewa wakati ambapo Ukraine na majirani zake wa Ulaya walikuwa wakisubiri kwa hamu maelezo ya mpango wake wa kumaliza vita nchini Ukraine, ambavyo Urusi ilianzisha kwa uvamizi wake mkubwa miaka mitatu iliyopita.
Ingawa rais huyo ametoa maelezo machache kuhusu jinsi amani inaweza kupatikana, malalamiko yake makubwa yamekuwa kwamba mataifa ya Ulaya hayajatoa msaada mkubwa kama Marekani, ambayo imechangia dola bilioni 175, na hivyo kuwa mfadhili mkubwa zaidi wa Ukraine.
Pia alisisitiza tena msimamo wake wa muda mrefu kwamba "tutamaliza vita hivyo vya kipuuzi."
China inatawala soko la kimataifa la madini adimu, ikiwa na haki za kuchimba madini hayo kwa asilimia 60 na kuzalisha hadi asilimia 90 ya ugavi wa dunia, kulingana na Taasisi ya Mafunzo ya Nishati ya Oxford.