Jaji Paige Whitaker anayesimamia kesi ya rapa Jeffery Lamar Williams maarufu Young Thug amesema kuwa muda wa majaribio wa rapa huyo hautabatilishwa, licha ya uwepo wa madai ya waendesha mashtaka kwamba amekiuka masharti ya makubaliano yake.
April 2,2025 Jimbo la Georgia liliwasilisha ombi la kufuta masharti ya kifungo cha nje kwa rapa Young Thug katika Mahakama Kuu ya Kaunti ya Fulton, Jimbo la Georgia, chini ya kesi namba 22SC183572, inayosimamiwa na Jaji Paige Whitaker. Taarifa hiyo ilikuwa na Kichwa cha Habari kinachosema “Ombi la Jimbo la Kufuta Masharti ya Kifungo cha Nje,” dhidi ya mshtakiwa, Jeffery Williams.
Ikumbukwe kuwa Rapa Young Thug aliruhusiwa kurudi nyumbani Novemba 1,2024 kwa masharti maalum akitumikia kifungo cha miaka 50 baada ya kukaa rumande kwa takribani miaka miwili bila dhamana tangu alipokamatwa Mei, 2022 akikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, ulanguzi wa dawa za kulevya na uendeshaji wa genge la wahuni.