Loading...

Hatari za kiafya kulala muda mchache baada ya kula

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

2 weeks ago
rickmedia: hatari-kiafya-kulala-muda-mchache-baada-kula-314-rickmedia

Katika maisha ya sasa, watu wengi wana ratiba zilizojaa shughuli nyingi, kiasi kwamba mara nyingi shughuli hizo huwa chanzo cha kurejea nyumbani usiku na kulala muda mfupi baada ya kula chakula.

Hilo linaweza kuonekana kama jambo la kawaida, lakini ni muhimu kuelewa athari zinazoweza kutokea endapo utalala muda mfupi baada ya kula chakula chako.

Wataalamu wa afya nchini Marekani wanasema muda mzuri wa kula chakula cha jioni kwa mtu yeyote ni kati ya dakika 180 (saa tatu) au dakika 240 (saa nne) kabla ya kupanda kitandani kulala. Kwa kufanya hivyo, wanasema kunaupa mwili nafasi ya kufanyia kazi chakula hicho kama inavyotakiwa.

Wataalamu hao wanasema saa tatu au nne kabla ya mtu kulala, ndiyo muda sahihi zaidi kwa kuwa mwili unaweza kukifanyia kazi chakula kama inavyotakiwa ikiwemo mmeng’enyo lakini pia kunamuepusha mtu kukumbana na magonjwa mbalimbali.

Utafiti huu unakazia ripoti ya Julai mwaka 2018 ambayo ilisema watu wanaokula chakula cha jioni kabla ya saa tatu usiku au angalau saa mbili kabla ya kulala wana hatari ya chini ya asilimia 20 kupata saratani ya matiti na kibofu, kuliko wale wanaokula chakula saa nne usiku au wale wanaokwenda kulala muda mfupi baada ya kula chakula.

Ushauri mwingine wa wataalamu umesema kunywa maji baada ya chakula ni muhimu kwa kila mtu. Lakini kila mmoja anapaswa kufanya hivyo angalau dakika 30 baada ya kumaliza kula chakula.