Sean "Diddy" Combs anakabiliwa na mashtaka mengine ya unyanyasaji wa kijinsia, yaliyowasilishwa na mwanamke mwingine anayejulikana kama Jane Doe, ambaye anadai kuwa alikuwa na umri wa chini ya miaka 18 wakati wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa nyaraka za kisheria zilizopatikana na TMZ, mwanamke huyo anasema tukio hilo lilitokea mwaka 2000 alipokuwa na umri wa miaka 16. Akiwa Manhattan baada ya kumaliza kazi ya kuangalia watoto, alikutana na Diddy na washirika wake wawili ndani ya SUV. Walimpa ofa ya kumpeleka nyumbani, lakini baada ya kushinikizwa na Diddy, alikubali kwa hofu.
Katika mashtaka hayo, anadai kuwa badala ya kumpeleka nyumbani, walimpeleka eneo tofauti. Anasema alipewa kinywaji na Diddy ambacho kilimfanya ajisikie usingizi na mlevi. Kisha anadai kuwa alibakwa na Diddy kabla ya kuachwa kwenye maeneo ya jengo alikoishi.
Timu ya wanasheria wa Diddy imekanusha madai haya mapya, wakitoa tamko:
"Haijalishi ni mashtaka mangapi yanawasilishwa, haitabadilisha ukweli kwamba Bwana Combs hajawahi kumbaka wala kufanya biashara ya binadamu — mwanaume au mwanamke, mtu mzima au mtoto. Tunaishi katika ulimwengu ambapo mtu yeyote anaweza kufungua kesi kwa sababu yoyote. Kwa bahati nzuri, kuna mfumo wa kisheria wa haki na usio na upendeleo wa kugundua ukweli, na Bwana Combs ana uhakika ataibuka mshindi mahakamani."
Mashtaka haya mapya yanaongeza changamoto zaidi kwa Diddy, ambaye tayari anakabiliwa na mashtaka mazito ya uhalifu yanayozidi 100.