Wakati Rais mteule wa Marekani, Donald Trump akisubiri kuapishwa Januari 20, mwaka huu, bado anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa wiki hii kwenye kesi yake ya kumlipa kahaba, baada ya jaji kukataa kusitisha hukumu yake licha ya mawakili wake kukata rufaa.
Katika kesi hiyo, Trump anatuhumiwa kumlipa Stormy Daniels ili kumziba mdomo kuhusu kuwapo kwa uhusiano kati yao.
Jaji wa Mahakama ya Manhattan, Juan Merchan, ameamuru usomwaji wa hukumu hiyo uendelee kama ulivyopangwa Ijumaa Januari 10, ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kuapishwa kwa Trump kuwa rais.
Jaji huyo amekataa shinikizo la mawakili wa Trump ambao wamekata rufaa kuitaka Mahakama ya Rufaa kuifuta hukumu ya awali, iliyomtia hatiani mteja wao.
Ikiwa hukumu hiyo itasomwa, Trump atakuwa rais wa kwanza kuchukua madaraka akiwa ametiwa hatiani kwa uhalifu.
Hata hivyo, Jaji Merchan ameandika kwamba hakuwa na nia ya kumhukumu Trump kifungo gerezani na kwamba hukumu ya "kuachiliwa bila masharti" ikimaanisha hakuna kifungo, faini ya fedha ingekuwa suluhisho linalowezekana zaidi."