"Leo tutachukua hatua ya kuwasimamisha kazi mara moja maofisa wote ambao wamejihusisha katika mahusiano ya kingono ndani ya ofisi za wizara za nchi.”
Hiyo ni moja ya kauli iliyochapishwa kupitia taarifa iliyotolewa kwenye X (zamani Twitter), na Makamu wa Rais wa Guinea ya Ikweta, Teodoro Nguema, akitangaza kuwachukulia hatua maofisa wa serikali hiyo wanaodaiwa kujihusisha na mahusiano ya kingono sehemu ya kazi, kisha kanda zao kuvuja.
Kiongozi huyo amesema serikali itachukua hatua kali dhidi ya vitendo hivyo, kwani ni ukiukwaji wa wazi wa kanuni za maadili na sheria ya maadili ya umma.
“Hatua hii ni hatua madhubuti katika sera yetu ya kutovumilia kabisa tabia zinazodhoofisha uadilifu wa huduma za umma. Maadili na heshima ni misingi muhimu katika utawala wetu, na hatutaruhusu tabia zisizowajibika kudhoofisha imani ya umma,” imeandika taarifa hiyo.
Kanda hizo zaidi ya 300 za ngono zinadaiwa kumuhusisha Baltasar Engonga, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Fedha (ANIF) nchini humo akiwa na wanawake kwa nyakati tofauti ndani ya ofisi ya umma.
Engonga anadaiwa kuonekana kwenye video hizo na wanawake, akiwemo mke wa kaka yake, mke wa mkuu wa usalama wa Rais, binamu yake na wengine.
Aidha, kanda hizo zilipatikana katika ofisi yake binafsi zikiwa zimechukuliwa kwa ridhaa na zimevuja mtandaoni, hali iliyoleta taharuki kwenye vyombo vya habari.
Engonga, ambaye ameoa na ana watoto sita, ameongoza shirika hilo lenye ushawishi mkubwa katika masuala ya uwazi wa kifedha na mfumo wa udhibiti wa nchi hiyo, likiwa na jukumu la kufanya uchunguzi wa kifedha na kudhibiti ufisadi.