Jeshi la Polisi kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Lugha Bashungwa(Mb) kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 66 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, Sura ya 223 na marejeo ya mwaka 2023 ametoa msamaha wa kutoshitakiwa kwa wamiliki wa silaha kinyume cha Sheria endapo watasalimisha silaha haramu kwa hiari kuanzia Septemba 1, 2025 hadi Oktoba 31, 2025
Kupitia Taarifa iliyotolewa leo Septemba 1, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi Msamaha huo ni moja ya juhudi na mikakati inayotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa Mikataba, Itifaki, Maazimio na Makubaliano mbalimbali ya Kuzuia Uzagaaji wa Silaha Ndogo na Nyepesi.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa mtu yeyote atakayepatikana na silaha baada ya kipindi cha msamaha yaani baada ya Mwezi Septemba na Oktoba, 2025 atakamatwa na kuchukuliwa hatua zingine za kisheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume na Sheria kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hiyo ya msamaha wa kutoshitakiwa uliotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pia, linawasisitiza wananchi wote ambao ndugu zao walikuwa wanamiliki silaha kihalali na wamefariki wahakikishe wanazisalimisha silaha hizo kulingana na masharti yaliyotajwa.