Watu 172 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, wakikabiliwa na mashitaka ya uharibifu wa mali, unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma moto, na kufanya maandamano bila kibali.
Kwa mujibu wa taarifa, makosa hayo yanadaiwa kufanyika kati ya Oktoba 29 na 30, 2025 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Watuhumiwa walifikishwa mahakamani Novemba 7, 2025, chini ya ulinzi mkali wa polisi na kusomewa mashitaka yao kwa makundi tofauti.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Jaines Kihwelo, akisaidiwa na Helen Mabula na Sara Heperias, alieleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wanakabiliwa na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287(a) cha Kanuni ya Adhabu, na mengine ya uharibifu wa mali kinyume na kifungu cha 326(1), pamoja na kuchoma moto kinyume na kifungu cha 319(a)(b).
Watuhumiwa wote wamekana mashitaka yanayowakabili na hawakupata dhamana kutokana na baadhi ya makosa hayo kuwa yasiyodhaminika. Mahakama imeamuru warejeshwe rumande hadi kesi hizo zitakapotajwa tena Novemba 17, 19 na 20, 2025.