Afisa wa polisi kutoka nchini Kenya amekamatwa kwa madai ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa amewekwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Rangwe, Kaunti ya Homa Bay.
Kulingana na ripoti ya polisi, John Mwangi ambaye alikuwa akiongoza zamu katika kituo hicho aliingia katika rumande saa tatu na nusu usiku wakati taa zikiwa zimezimwa na alipomfikia alimshika shingo msichana huyo na kumlazimisha avue nguo zake kwa nguvu, kisha kumbaka.
“Wakati wa tukio hilo, mwenzake Tonny Oketch alikuwa ameenda kuchukua mshumaa kutoka nje ya eneo hilo kwani eneo lilikuwa giza," ilisomeka ripoti ya polisi.
Baada ya askari hao kubadilishana zamu asubuhi, mwathiriwa alimjulisha Afisa Oketch kuhusu tukio hilo na kisha taarifa hiyo ikamfikia OCS ambaye alianzisha uchunguzi wa haraka na mtuhumiwa kukamatwa.