RC Chalamila ashiriki uzinduzi wa duka la kisasa la Airtel

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

1 hour ago
rickmedia: chalamila-ashiriki-uzinduzi-duka-kisasa-airtel-503-rickmedia

Airtel Tanzania imezindua duka maalumu la kisasa katika jengo la makao makuu yake jijini Dar es Salaam, ikiimarisha mkakati wake wa Airtel Kila Kona wa kusogeza huduma za mawasiliano, kidijitali na kifedha karibu zaidi na wateja.

Duka hilo limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, na linatoa huduma za intaneti, Airtel Money, intaneti ya nyuzi za mawasiliano (fibre) kwa matumizi ya nyumbani na biashara, suluhisho za kidijitali kwa kampuni na taasisi, usajili wa laini na huduma kwa wateja, vyote vikiwa vinapatikana katika eneo moja.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Chalamila alisema, “Mawasiliano ya uhakika si anasa kwa Dar es Salaam; ni nyenzo muhimu kwa biashara na ukuaji wa uchumi. Tunaipongeza Airtel kwa uwekezaji wake katika miundombinu ya kidijitali na tunaitaka kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa watanzania ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi wetu.”

Chalamila pia aliipongeza Airtel kwa uwekezaji wake katika teknolojia za mawasiliano za 4G na 5G, huku akihimiza kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa watanzania na kuhakikisha wateja wanapata msaada wenye ufanisi.

Pia alisisitiza mchango wa Airtel katika uchumi wa taifa kupitia ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania, ambayo inamiliki asilimia 49 ya hisa za kampuni hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema duka hilo linaakisi dhamira ya kampuni ya kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora huku ikichangia fursa za ajira, ujasiriamali na ujumuishaji wa kidijitali.

Kamoto alisema kwa mwaka huu 2026, Airtel imelipa gawio la shilingi billioni 65.48 kwa serikali, na kufanya jumla ya gawio lililolipwa kwa Serikali kufikia takribani shilingi bilioni 350 tangu mwaka 2019.

Airtel imeanzisha zaidi ya maduka 95 nchini kote, sambamba na matawi ya Airtel Money na maelfu ya mawakala, hatua inayopanua wigo wa upatikanaji wa huduma zake kwa wateja katika maeneo mbalimbali ya nchi, kwa kuzingatia dhamira yake ya Airtel Kila Kona.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Adriana Lyamba, alisema duka hilo linaunganisha teknolojia za kisasa za kidijitali na usanifu unaozingatia utunzaji wa mazingira ili kuboresha utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Airtel.

“Duka hili ni tofauti na maduka yetu mengine. Hili ni duka maalumu la kisasa la kidijitali lililoundwa ili kuwapatia wateja wetu huduma zenye viwango vya kimataifa. Pia limezingatia utunzaji mazingira na matumizi bora ya teknolojia, ikiwa ni sehemu ya dhamira yetu ya kujenga biashara endelevu yenye manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Lyamba.

Aliongeza kuwa Airtel inaendelea kuwekeza kwa watu, teknolojia na miundombinu ili kufikia matarajio na kuboresha huduma kwa wateja.

Uzinduzi wa duka hilo unaimarisha dhamira ya Airtel Tanzania ya kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kidijitali, kusaidia biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.