Makundi yanayompinga Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, yameungana chini ya jukwaa jipya la kisiasa na kijeshi linaloitwa Front pour la refondation de la Nation (FRN), lililotangazwa mjini Goma baada ya kutangazwa kuvunjwa kwa Alliance Fleuve Congo (AFC).
Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila Kabange, ametajwa kuongoza jukwaa hilo, akiwa na Bertrand Bisimwa na Corneille Nangaa kama manaibu wake, huku Jenerali Sultani Makenga akiteuliwa kuwa mkuu wa jeshi na daktari Freddy Kaniki kuwa katibu mkuu.
Tamko la kuanzishwa kwa jukwaa hilo lilisomwa na Claude Ibalanki, aliyesema kuwa AFC inafikia mwisho na nafasi yake inachukuliwa na FRN, ambayo inalenga kuunganisha makundi yanayompinga Rais Tshisekedi.
Tangazo hilo limeibua maoni tofauti miongoni mwa wananchi wa Kongo, huku baadhi wakisema limethibitisha nafasi ya Kabila katika mgogoro wa mashariki mwa nchi hiyo, wakati mtetezi wa haki za binadamu, Philemon Ruzinge, akionya kuwa muungano huo unaweza kuongeza hatari ya usalama nchini.
Kwa upande wake, seneta wa zamani Moïse Nyarugabo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Kabila, amewataka wananchi kuungana na kujiunga na FRN, akisema Kongo inahitaji kuokolewa kutokana na hali inayozidi kuzorota.