Gwiji wa muziki wa Hip-Hop, Jay-Z, na mwanamuziki nguli wa R&B, Alicia Keys, wanatarajiwa kukiwasha New York hadi California pale watakapopanda jukwaani show ya Super Bowl LXI Halftime Show mwaka 2027.

Kwa mujibu wa tovuti ya Page Six, Alicia Keys amekuwa kwenye mazungumzo na rapa huyo mzaliwa wa Brooklyn ili kuungana naye kwenye uwanja wa SoFi Stadium uliopo Inglewood, California, usiku wa mchezo huo mkubwa utakaofanyika tarehe 14 Februari, 2027. Aidha, jina la mwimbaji John Legend nalo linatajwa kama mmoja wa wasanii wanaoweza kupanda jukwaani siku hiyo.

Wasanii wote wawili (Alicia Keys na John Legend) wanasimamiwa na kampuni ya Roc Nation inayomilikiwa na Jay-Z, ambayo pia ndiyo inayohusika na utayarishaji wa onyesho hilo la Super Bowl. Ukaribu wao kikazi na Jay-Z ni wa muda mrefu; mwezi Oktoba 2026, John Legend alipanda jukwaani na Jay-Z katika uwanja huohuo wa SoFi kutumbuiza wimbo wa "God Did" wakati wa kufunga ziara yake ya maadhimisho ya miaka 30 (Jay-Z 30).

Kwa upande wake, Alicia Keys alishirikiana na Jay-Z kwenye wimbo wake wenye mafanikio makubwa zaidi kibiashara, "Empire State of Mind", wimbo ambao umekuwa kama wimbo wa taifa wa jiji la New York katika karne ya 21.
Hatua hii inakuja mara tu baada ya Jay-Z kutangazwa rasmi kuwa msanii mkuu (headliner) wa onyesho la 2027 Apple Music Super Bowl LXI Halftime Show, muda mfupi baada ya kumaliza ziara yake ya viwanja vikubwa.