Dkt. Mwigulu Nchemba amethibishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupigiwa Kura za ndiyo 369 kati ya kura 371 zilizopigwa leo Novemba 13, 2025.
Waziri Mkuu Mteule, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoingia katika awamu yake ya pili ina kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025–2050, ambayo inalenga kuleta mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akitoa hotuba ya shukrani mara baada ya Bunge kumuidhinisha kwa kura nyingi kushika nafasi ya Waziri Mkuu, Dkt. Nchemba amesema Dira hiyo inaweka kipaumbele kwenye masuala ya ajira, ambapo lengo ni kutoa ajira milioni nane kwa vijana nchini.
Amesema anatambua changamoto ya ajira kwa vijana na ameahidi kushirikiana kwa karibu na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ajira zinapatikana na umasikini unaokadiriwa kufikia asilimia 26 unapungua kwa kiwango kikubwa.