WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwasisitiza Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili amani, upendo, ustahimilivu na mshikamano viendelee kudumu nchini.
Amesema hayo leo (Jumapili, Novemba 16, 2025) alipowasilisha salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kisasa, Mkoa wa Dodoma.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawasalimu sana. Yuko pamoja nanyi, na rai yake kwa Watanzania wote ni kuendelea kufanya maombi kwa ajili ya Taifa letu ili liendelee kuwa tulivu.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kulindwa na kuenziwa, kwa sababu pasipo amani, Taifa halitoweza kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendesha ibada na shughuli nyingine za kijamii.
“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu mengine yeyote, pasipo amani hatuwezi kuendesha ibada. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuiombea nchi yetu. Pakiwa na amani tunaweza kutekeleza yale yaliyo katika matarajio yetu, tunaweza hata kutatua yale tunayoyaona kuwa ni magumu.”