Mzee Clemence Mwandambo anashikiliwa na jeshi la Polisi Jijini Mbeya

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

2 hours ago
rickmedia: mzee-clemence-mwandambo-anashikiliwa-jeshi-polisi-jijini-mbeya-943-rickmedia

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Clemence Mwandambo, mkazi wa Mtaa wa Uzunguni “A” ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Awali ya Saint Clemence, jijini Mbeya, kwa tuhuma za kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo pamoja na kukashfu imani za dini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ni kwamba mtuhumiwa amekamatwa jana Disemba 29, majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Uzunguni, jijini Mbeya.

Inadaiwa kuwa Mwandambo alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kuchapisha na kusambaza maudhui yanayodaiwa kukashfu imani za dini ya Kiislamu na Kikristo, pamoja na taarifa zinazodaiwa kuwa za uongo.

“Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa kina ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kabla ya kuchukua hatua zaidi za kisheria dhidi ya mtuhumiwa,”amesema Kamanda Kuzaga.

Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia sheria, maadili na kuheshimu imani za watu wengine, huku wakisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria.