Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limethibitisha tukio la kusikitisha la kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aitwaye Ramin Sahbdad, mkazi wa Kata ya Mpela, Manispaa ya Tabora. Mtoto huyo alipotea tangu Julai 18, 2025, na juhudi za kumtafuta zilikuwa zikiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Polisi, mwili wa mtoto huyo uligundulika ukiwa unaelea juu ya maji ya kisima kilichopo nyumbani kwao, mnamo Julai 20, 2025. Baada ya mwili huo kupatikana, familia ilifanya mazishi yake jioni ya siku hiyo hiyo.
Polisi wanasema uchunguzi wa awali unaendelea ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo, ikiwa ni pamoja na iwapo kuna dalili zozote za uzembe, ajali, au uhalifu wowote unaohusiana na tukio hilo.
Tukio hili limeibua huzuni na simanzi kubwa kwa familia, majirani, na jamii nzima ya Mpela, huku wakazi wakitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini zaidi katika uangalizi wa watoto wao, hasa nyakati wanapocheza maeneo ya nyumbani.