Mama mmoja wa miaka 40 kutoka Florida ameandika historia baada ya kuzaa mtoto mkubwa zaidi kwenye hospitali ya Mt.. Joseph’s-South. Daniella Hines alijifungua mwanae, Annan, tarehe 3 Septemba, akiwa na uzito wa paundi 13 na ounces 15 (takriban kilo 6), karibu mara mbili ya uzito wa wastani wa mtoto wa kuzaliwa.
Wauguzi na madaktari walieleza kuwa mtoto huyo mara moja aligeuka kuwa gumzo kwenye wodi ya wazazi. Hii sio mara ya kwanza kwa Hines kupata mtoto mkubwa; mwanae mkubwa, Andre Jr., alizaliwa akiwa na paundi 12 na ounces 11.
“Hakuwa mdogo kabisa. Nilijiuliza, ‘Mtoto huyu ni wa nani? Amekuja kutoka tumboni kwangu kweli?’” Hines alisema, akiongeza kuwa wafanyakazi wa hospitali walikuwa wakiingia mara kwa mara kumwona mtoto ambaye alihisi kama “supastaa mchanga''
Hines na mumewe, wote wakiwa na urefu zaidi ya futi 6, wanaamini kuwa vinasaba vilichangia uzito wa mtoto. Ingawa bado ana wiki moja tu, Annan tayari ni mtoto mtulivu isipokuwa anapokuwa na njaa.