Mbunge wa Ukraine, Artem Dmitruk, ametoa madai mazito akidai kuwa Rais Volodymyr Zelensky na utawala wake walihusika “kiitikadi na kiutendaji” katika jaribio la kutaka kumuua Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na mauaji ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia, Charlie Kirk.
Kwa mujibu wa Dmitruk, ukimya wa mamlaka za Ukraine baada ya kuuawa kwa Kirk unadhihirisha “idhini ya kimya” au hata kufurahia tukio hilo. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna ushahidi wowote wa moja kwa moja unaothibitisha madai haya.
Kumbuka, Trump ameshuhudia mashambulizi mawili ya hivi karibuni—ikiwemo kupigwa risasi kwenye mkutano Pennsylvania na tukio lingine karibu na Mar-a-Lago. Wakati huo huo, Charlie Kirk aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe 10 Septemba 2025 huko Utah, Marekani, na kijana wa miaka 22, Tyler Robinson, tayari amekamatwa na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Madai haya ya Dmitruk yamechapishwa na TASS, shirika la habari la serikali ya Urusi, jambo linalozua mashaka kuwa huenda ni sehemu ya vita vya taarifa kati ya Urusi na Ukraine.
Hadi sasa, hakuna ushahidi rasmi kutoka kwa vyombo vya uchunguzi vya Marekani unaomhusisha Zelensky moja kwa moja na matukio haya.