Mahakama kumaliza ubishi nyaraka ya malipo ya mkopo wa Equity leo

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

4 months ago
rickmedia: mahakama-kumaliza-ubishi-nyaraka-malipo-mkopo-equity-leo-201-rickmedia

Hatima ya uhalali wa nyaraka iliyopingwa katika kesi ya kibiashara iliyofunguliwa na Kampuni ya Continental Reliable Clearing (T) Limited (CRC) dhidi ya Benki za Equity Tanzania na Equity Kenya, itajulikana leo Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo.

Kampuni hiyo ilifungua kesi hiyo baada ya benki ya Equity Kenya kupitia wakala wake, Equity Tanzania kuiandikia barua ikiipa siku 21 kurejesha mkopo ambao zilikuwa zimeipatia kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013, Dola za Marekani 10,139,664.95 (yaani Dola 10.13 milioni, sawa na zaidi ya Sh26 bilioni)

Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023 inayosikikizwa na Jaji Dk Agatho Ubena, CRC inadai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.

Jana kampuni hiyo kupitia shahidi wake wa pili, Alexander Johns akiongozwa na wakili wa kampuni hiyo, Frank Mwalongo, iliiomba mahakama hiyo ipokee nyaraka hiyo ambayo ilidaiwa kuwa ni jedwali la malipo ya mkopo wote ambao kampuni hiyo ilipewa na benki hizo.