Mtandao wa kijamii wa TikTok umeondoa zaidi ya video 500,000 nchini Kenya katika kipindi cha miezi mitatu, kufuatia ukiukaji wa kanuni za jamii za jukwaa hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji wa kanuni za jamii kwa robo ya pili ya mwaka 2025, TikTok ilisema kuwa jumla ya video 592,037 zilifutwa kati ya Aprili na Juni mwaka huu. Kati ya hizo, zaidi ya asilimia 92.9 zilitambuliwa na mfumo wa kiotomatiki na kuondolewa kabla ya kutazamwa na watumiaji, huku asilimia 96.3 zikifutwa ndani ya masaa 24 tangu kupakiwa.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye kiwango kikubwa cha maudhui yanayokiuka sera za jukwaa hilo, ikilinganishwa na nchi jirani kama Uganda na Tanzania.
Kwa kiwango cha kimataifa, TikTok iliondoa zaidi ya video milioni 189 katika kipindi hicho, sawa na takriban asilimia 0.7 ya jumla ya video zote zilizopakiwa ulimwenguni.