Afungwa Miaka 20 Jela kwa Kosa la Shambulio la Aibu

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

8 hours ago
rickmedia: afungwa-miaka-jela-kwa-kosa-shambulio-aibu-226-rickmedia

Mahakama ya Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, Agosti 18, 2025 imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 20 Jela kwa mtuhumiwa Idd Omary Shelugwaza mwenye umri wa miaka 26, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kwakibuyu, Kata ya Kipumbwi, Tarafa ya Mwera, Wilaya ya Pangani, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la shambulio la aibu dhidi ya mtoto mwenye umri wa miaka 4.

Awali, ilielezwa mahakamani kuwa mnamo tarehe 24 Juni 2025 huko Kijiji cha Kwakibuyu, mtuhumiwa alitenda kosa hilo dhidi ya mtoto huyo mwenye umri wa miaka Minne mwanafunzi na mkazi wa kijiji hicho. Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Pangani ambapo mtuhumiwa alikamatwa huku uchunguzi wa shauri hilo ulianza mara moja.

Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani kwa namba 15855/2025 na kupelekwa mbele ya Mheshimiwa Hakimu Francisca Magwiza - SRM. Baada ya kusomewa shtaka, mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo, na shauri liliendelea kwa mashahidi mbalimbali kutoa ushahidi wao mahakamani.

Akisoma hukumu tarehe 18 Agosti 2025, Hakimu Magwiza alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na hivyo kumpata mtuhumiwa na hatia ya shambulio la aibu, na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela ili iwe fundisho kwa jamii na kulinda haki za watoto.