Umoja wa Afrika (AU) umeunga mkono kampeni ya kimataifa ya kuachana na ramani ya Mercator ya karne ya 16 na kutumia ramani inayoonyesha ukubwa halisi wa Afrika. Ramani ya Mercator huongeza maeneo ya karibu na ncha za dunia na kupunguza yale yaliyo karibu na ikweta, hivyo kuifanya Afrika ionekane ndogo kuliko ilivyo.
Naibu Mwenyekiti wa Tume ya AU, Selma Malika Haddadi, alisema ramani hiyo inaonesha Afrika kama “marginal” licha ya kuwa bara la pili kwa ukubwa duniani lenye zaidi ya watu bilioni moja. Kampeni ya “Correct The Map” inayoongozwa na Africa No Filter na Speak Up Africa inalenga shule, serikali na mashirika ya kimataifa zitumie ramani ya Equal Earth iliyozinduliwa mwaka 2018.
Hadi sasa, ombi la mapitio lipo mbele ya shirika la Umoja wa Mataifa la geospatial (UN-GGIM) likiwa na uungwaji mkono kutoka kwa jumuiya kama CARICOM. Viongozi wa kampeni wanasema upotoshaji huu unaathiri fahari ya Waafrika, hasa watoto shuleni. Tayari taasisi kama Google Maps na Benki ya Dunia zimeanza kutumia mbadala wa Mercator, ishara kuwa mabadiliko yanaendelea.