Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo Jumanne, Januari 20, 2025 kufuatia kifo cha mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Mzee Mtei ambaye ni mwanzilishi wa Chadema na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, nyumbani kwake Tengeru, jijini Arusha.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia imeeleza, “chama kinatangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera za chama zitapepea nusu mlingoti.”
Brenda amesema Mzee Mtei amefariki dunia siku moja kabla ya Chadema hakijaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ambapo Januari 21, 1993, Mzee Mtei alikabidhiwa cheti cha usajili wa chama hicho.
Chadema imesema taarifa zaidi za maombolezo, kuaga mwili na mazishi zitatolewa baadaye leo.