Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’imepanda kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mujibu wa chati ya mwezi Januari 2026 iliyotolewa juzi.
Kutinga hatua ya 16 bora ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizofikia tamati huko Morocco juzi Jumapili, kumeonekana kuibeba Taifa Stars ambayo imepaa kutoka nafasi ya 112 hadi nafasi ya 110 ikiwa na pointi 1186.14.
Katika fainali hizo za AFCON 2026, Taifa Stars ilitoka sare katika mechi mbili na kupoteza michezo miwili, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
Wakati Taifa Stars ikipanda, mambo hayajaenda vizuri kwa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo imeporomoka kwa nafasi tatu kutoka ile ya 85 hadi katika nafasi ya 88.
Katika fainali za AFCON 2025, Uganda iliishia katika hatua ya makundi baada ya kuchapwa mechi mbili na kutoka sare moja.
Historia imeandikwa na Morocco ambayo kufanya kwake vizuri katika AFCON 2025 ambapo iliishia fainali, kumeibeba na kuipandisha kwa nafasi tatu.