Msanii maarufu wa vichekesho, Asma Majid, amepeleka kesi mahakamani akiwataka wanamitandao maarufu Juma Lokole, MAIMARTHA Jesse, na Mbarouk Khan — kumlipa fidia ya Shilingi milioni 500 kwa madai ya kuchapisha taarifa za uongo zinazomhusisha na harusi ya mtangazaji Ally Kamwe, iliyofanyika tarehe 1 Agosti.
Katika madai hayo, Asma anasema kuwa taarifa hizo za mtandaoni zimemsababishia madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na kudhalilika kijamii, kupoteza heshima na kuathiri taswira yake kama mtu wa umma.
Asma anasisitiza kuwa hakuhusiana kwa namna yoyote na tukio hilo la harusi, na kwamba taarifa zilizosambazwa mtandaoni ni za kupotosha na kumharibia jina makusudi. Anadai kuwa vitendo hivyo vinakiuka haki zake za msingi na vinavunja sheria za mawasiliano na makosa ya mtandao.
Kesi hiyo inatazamiwa kufuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali wa sanaa na mitandao ya kijamii, huku ikifungua mjadala kuhusu mipaka ya uhuru wa kutoa maoni mitandaoni na ulinzi wa hadhi ya watu maarufu.