Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara limesema limemkamata Anastanzia Exavery Mahatane (27), maarufu Ebitoke katika fukwe za Msanga Mkuu, Mjini Mtwara akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na wala hakuwa ametumbukizwa katika shimo wala kutekwa kama ambavyo alieleza mitandaoni.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa Julai 30, 2025 Ebitoke, ambaye ni Msanii wa vichekesho anayeishi katika Kata na Kijiji cha Msanga Mkuu Wilaya ya Mtwara, alichapisha taarifa katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kuwa yeye kwa sasa yupo Mtwara na kwamba ametumbukizwa katika shimo huko katika fukwe za Msanga Mkuu na kwamba wapo watu ambao aliwataja kwa majina kuwa wanataka kumuua.
Jeshi la Polisi limesema lilianza uchunguzi wa haraka ili kujua ukweli wa taarifa hiyo, na katika uchunguzi wa awali, lilibaini kwamba Ebitoke alifika Mtwara tangu Aprili 2025 na kufikia katika hoteli moja iliyopo Msanga Mkuu na kisha kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake kumwendea vibaya huko alikokuwa.
"July 31, 2025 saa 11:00 jioni Jeshi la Polisi Mtwara lilimkamata Anastazia Mahatane Ebitoke huko katika fukwe za Msanga Mkuu akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya matibabu," imesema taarifa hiyo.