Mjane wa bilionea marehemu Reginald Mengi, Bi. Jacqueline Mengi, amemuandikia barua ya wazi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akieleza changamoto na dhuluma wanazokumbana nazo wake na watoto baada ya kifo cha baba wa familia, hasa katika masuala ya mgawanyo wa urithi.
Kupitia barua hiyo, Jacqueline amesisitiza kuwa hali hiyo si ya kipekee kwake bali imeenea kwa familia nyingi nchini, ambapo wajane na watoto hukosa haki zao za msingi baada ya msiba wa baba.
Bi. Jacqueline ameiomba Serikali kuingilia kati kwa kuweka mfumo madhubuti wa kisheria na kijamii utakao linda haki za watoto na wajane, ili kuepusha vitendo vya unyanyasaji, uvamizi wa mali, na migogoro ya kifamilia inayoibuka mara kwa mara.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini, jamii, na asasi za kiraia kushirikiana katika kulinda utu na haki za wanawake na watoto, hasa katika kipindi kigumu cha maombolezo na baada ya msiba.
Barua hiyo imeibua mjadala mpana katika jamii kuhusu haki za urithi, nafasi ya wanawake, na umuhimu wa kuwa na maandalizi ya kisheria mapema ili kuepuka migogoro.