Madagascar Yatangaza Marufuku ya Kutoka Nje Usiku Kufuatia Maandamano ya Kupinga Mgao wa Umeme na Maji

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

1 day ago
rickmedia: madagascar-yatangaza-marufuku-kutoka-nje-usiku-kufuatia-maandamano-kupinga-mgao-umeme-maji-426-rickmedia

Serikali ya Madagascar imetangaza marufuku ya kutoka nje usiku kote nchini, kufuatia maandamano makubwa yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu, Antananarivo, kupinga mgao wa umeme na maji unaoendelea.

Maandamano hayo yamechochewa na hasira za wananchi kuhusu huduma duni za kijamii, hasa kukatika kwa umeme na maji kwa muda mrefu. Waandamanaji waliripotiwa kuziba barabara kwa kutumia matairi yanayowaka moto na mawe, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa usafiri na shughuli za kila siku.

Vikosi vya usalama vililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji, huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda katika maeneo kadhaa ya jiji.

Taarifa kutoka kwa maafisa wa usalama pia zimethibitisha kuwepo kwa matukio ya uporaji, ambapo baadhi ya maduka na benki zilivunjwa na kuporwa mali. Serikali imelaani vikali vitendo hivyo na kuahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.

Marufuku hiyo ya kutoka nje usiku inaanza kutekelezwa mara moja kuanzia saa 1 usiku hadi saa 11 alfajiri, hadi hali ya usalama itakaporejea kuwa ya kawaida.

Serikali imewataka wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya dola katika kudumisha amani, huku ikiahidi kufanya juhudi za kutatua changamoto za huduma za umeme na maji.