Msemaji wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) ameeleza kwa Mail Online kwamba Lame, ambaye ni raia wa Italia aliyezaliwa Senegal, alizuiliwa na shirika hilo mnamo Juni 6 kutokana na "ukiukaji wa sheria za uhamiaji" baada ya kuingia Marekani tarehe 30 Aprili.
Khaby, ambaye jina lake kamili ni Seringe Khabane Lame, alipewa ruhusa ya kuondoka nchini kwa hiari na tayari ameondoka Marekani.
"Tulimzuia Seringe Khabane Lame, mwenye umri wa miaka 25, raia wa Italia, tarehe 6 Juni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harry Reid, Las Vegas, Nevada, kwa ukiukaji wa sheria za uhamiaji. Lame aliingia Marekani tarehe 30 Aprili na alikaa zaidi ya muda ulioruhusiwa na visa yake. Aliruhusiwa kuondoka kwa hiari tarehe 6 Juni na sasa ameondoka nchini," ICE ilisema.
Tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipochukua tena madaraka mnamo Januari, amekuwa akitekeleza kampeni kubwa ya kuwafukuza raia wasiokuwa na vibali halali nchini Marekani.
ICE imekuwa ikifanya misako karibu kila siku tangu Trump arejee Ikulu. Maelfu kwa maelfu ya watu walioko nchini Marekani kinyume cha sheria wamekamatwa na kufukuzwa nchini tangu wakati huo.
Khaby, ambaye anajulikana kwa jina la mtandaoni @khaby.lame, alihamia kutoka Senegal kwenda Chivasso, karibu na jiji la Turin nchini Italia akiwa na umri wa mwaka mmoja. Alipata uraia rasmi wa Italia mwaka 2022.