Mwanamuziki maarufu wa R&B, R. Kelly, anaripotiwa kuwa katika hali ya taharuki na uwoga mkubwa akiwa gerezani, ambapo amedaiwa kuangua kilio na kuomba kwa dhati aachiliwe, akieleza kuwa maisha yake yako hatarini na afya yake inazidi kudorora.
Kwa mujibu wa ripoti ya TMZ, wakili wake Nicole Blank Becker amesema kuwa msanii huyo mwenye umri wa miaka 58 alipiga simu akiwa gerezani kwa hisia, akihofia hali ya maisha aliyonayo sasa tangu arudishwe guerezani baada ya kutoka hospitalini.
R. Kelly kwa sasa anazuiliwa katika Kitengo Maalum cha Gereza (Special Housing Unit) kilichoko katika gereza moja huko North Carolina, hali ambayo Becker anasema imeongeza wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa msanii huyo.
Wakili huyo ameongeza kuwa Kelly anaishi kwa hofu kila siku, akihisi kutengwa na kutotendewa haki, na kwamba hali ya afya yake kimwili na kiakili inazidi kuzorota akiwa kizuizini.
Kelly, ambaye amehukumiwa kwa makosa mbalimbali ya unyanyasaji wa kingono, amekuwa akikata rufaa mara kwa mara kutaka kuachiliwa kwa sababu za kiafya na kiusalama, lakini bado anasalia gerezani akisubiri hatua zaidi za kisheria.