Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) raia wa China, alietajwa kama miongoni mwa wabakaji wabaya zaidi nchini Uingereza, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuwalewesha na kuwabaka wanawake angalau 10 nchini Uingereza na China.
#ZhenhaoZou, mwenye umri wa miaka 28, alipokea hukumu ya kifungo cha maisha siku ya Alhamisi katika Mahakama ya Crown ya Inner London, akiwa na kifungo cha chini cha miaka 24 kabla ya kustahili kuomba msamaha wa kifungo.
Jaji Rosina Cottage alisema Zou atatumikia miaka 22 na siku 227 kabla ya kuzingatiwa kwa msamaha, kutokana na muda ambao tayari ameutumikia rumande, kwa mujibu wa PA Media.
#Zou alipatikana na hatia mwezi Machi kwa makosa 11 ya ubakaji, kosa moja la kumfunga mtu kinyume cha sheria, makosa matatu ya kutazama watu kimapenzi kwa siri (voyeurism), pamoja na makosa mengine, ikiwa ni pamoja na kumiliki maudhui ya ponografia na dawa ya kulevya kwa nia ya kutekeleza uhalifu wa kingono.
Waendesha mashtaka walisema wahanga wengi walileweshwa hadi kupoteza fahamu na kuachwa bila ulinzi kabla ya kushambuliwa.
Kwa mujibu wa mamlaka, Zou ambaye pia alitumia jina la utani “Pakho” mtandaoni—aliwalenga wanawake, wengi wao wakiwa wanafunzi wa asili ya Kichina, kupitia WeChat na programu mbalimbali za kutafuta wapenzi. Aliwavuta hadi kwenye vyumba vya kupanga mjini London na China, ambako aliwalewesha, kuwabaka, na katika baadhi ya matukio, kuwaibia vitu vyao vya thamani kama vito na nguo.
Polisi walisema Zou alirekodi baadhi ya mashambulizi hayo kwa kutumia simu za mkononi na kamera zilizofichwa. Huduma ya Mashtaka ya Umma (Crown Prosecution Service - CPS) ilimwelezea kama mnyanyasaji wa hila aliyewinda wanawake "kwa njia ya woga sana."
Zou alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha University College London (UCL) alipokamatwa mwezi Januari 2024 baada ya mmoja wa waathirika wake kujitokeza. Wachunguzi baadaye waligundua ushahidi zaidi unaomhusisha na mashambulizi katika nchi zote mbili.
Mamlaka zina hofu kuwa idadi halisi ya waathirika inaweza kuwa kubwa zaidi. Mwezi Machi, polisi wa Uingereza walisema wanaamini Zou huenda alibaka zaidi ya wanawake 50, kwani waathirika zaidi waliendelea kujitokeza.
Katika taarifa yao, waendesha mashtaka waliwasifu manusura kwa kuwaita “wenye nguvu na ujasiri wa kipekee,” na kuongeza, “Hakika ujasiri wao wa kujitokeza ndiyo uliopelekea hukumu hii kupatikana.”