Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo mkoani Dodoma imefanya upasuaji wa kuweka mlango wa bandia kwenye moyo wa mgonjwa na hivyo kuwa hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma hiyo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa BMH, Ahmed Toure amesema upasuaji huo unafanyika pale mlango wa kwenye moyo unapokuwa umeziba.
"Hivyo tumetoa mlango ulioziba ambao kitaalamu unaitwa valve na kuweka mlango wa bandia ili kuruhusu damu kuendelea kupita," amesema Dkt. Toure.
Upasuaji huo umefanyika kwenye kambi ya pamoja ya matibabu ya moyo kati ya madaktari wa BMH kwa kushirikiana na wenzao kutoka Uholonzi.
Mlango huo unapobadilishwa mgonjwa anapona tatizo lililokuwa linamsumbua la mlango kuziba na damu itapita vizuri kama zamani.