Takriban watu sita wameuwawa na saba kujeruhiwa katika shambulio la anga la Israel kwenye jengo la ghorofa huko Beirut usiku wa kuamkia leo, Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema Alhamisi, wakati serikali mbalimbali ulimwenguni zikihangaika kuwahamisha raia wao kutoka nchi hiyo. Shambulio hilo la anga lilipiga karibu na makazi ya mji mkuu wa wilaya ya Bashoura.
Wakazi waliripoti harufu kama ya salfa kufuatia shambulio hilo, na Shirika la Habari la Taifa la Lebanon liliituhumu Israel kwa kutumia mabomu ya fosforasi, ambayo yamepigwa marufuku na sheria za kimataifa kutumika karibu na raia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu siku za nyuma yaliishutumu Israel kwa kutumia makombora ya fosforasi katika miji na vijiji vilivyokumbwa na vita kusini mwa Lebanon.