Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha imemhukumu kifungo cha maisha jela Stephano Anyosisye Mwasala (35), aliyekuwa mmiliki wa kituo cha kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kiitwacho Majest Children Home, mkazi wa Msongola, Kibaha kwa kosa la kuanzisha kituo hicho bila kuwa na leseni, kubaka na kuwanyanyasa kingono watoto saba, kati ya waliokuwa akiwalea.
Imeelezwa kuwa, kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 2024 na Januari 2025 huko Msongola katika kituo hicho, mshtakiwa alikuwa akiwaingilia kimwili na kuwafanyia vitendo vya kingono watoto hao saba wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 14.
Upande wa Jamhuri umeieleza mahakama kuwa, Jeshi la Polisi mara baada ya kupata taarifa hizo kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na upelelezi uliendelea kisha mtuhumiwa alifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.