Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa Venezuela imekubali kutoa kati ya mapipa milioni 30 hadi 50 ya mafuta kwa nchi hiyo, hatua aliyoeleza inalenga kunufaisha wananchi wa nchi zote mbili.
Mafuta hayo yatauzwa kwa bei ya soko la kimataifa, huku mapato yatakayopatikana yakisimamiwa na Marekani ili kuelekezwa kwenye matumizi yanayodaiwa kuwa ya manufaa kwa raia wa Venezuela na Marekani.
Kupitia ujumbe alioutoa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump amesema mpango huo ni sehemu ya hatua za haraka kufuatia mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Venezuela baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Nicolás Maduro.
Ameeleza kuwa ametoa maelekezo kwa Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, kuanza mara moja utekelezaji wa mpango huo kwa kusafirisha mafuta hayo kupitia meli maalumu hadi katika bandari za Marekani.
Trump amesisitiza kuwa udhibiti wa mapato ya mauzo ya mafuta hayo utafanywa na serikali yake, ili kuhakikisha fedha hizo hazipotei wala kutumika vibaya. Kwa mujibu wa rais huyo, lengo ni kurejesha uthabiti wa kiuchumi wa Venezuela huku pia Marekani ikihakikisha upatikanaji wa nishati kwa gharama nafuu katika kipindi cha misukosuko ya soko la dunia.
Aidha, Trump amebainisha kuwa Marekani inapanga kushirikiana na kampuni kubwa za mafuta za Kimarekani, zikiwemo ExxonMobil, Chevron na ConocoPhillips, katika kuifufua sekta ya mafuta ya Venezuela, iliyodhoofika kwa miaka kadhaa kutokana na vikwazo vya kiuchumi, ukosefu wa uwekezaji na migogoro ya kisiasa.