Petroli na mafuta ya taa bei juu huku Dizeli yabaki palepale

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

1 day ago
rickmedia: petroli-mafuta-taa-bei-juu-huku-dizeli-yabaki-palepale-151-rickmedia

Watumiaji wa mafuta ya petroli na mafuta ya taa nchini watalazimika kutumia fedha zaidi kupata lita moja ya mafuta baada ya bei kuongezeka, wakati watumiaji wa dizeli wakipata ahueni.

Hiyo ni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia Jumatano, Januari 7, 2026 saa 6:01 usiku.

Wakati ongezeko na kushuka kwa bei kukishuhudiwa nchini, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 4.26 kwa mafuta ya petroli, asilimia 12.83 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 10.44 kwa mafuta ya taa.

Bei hiyo imepungua pia wakati ambao gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.1 kwa mafuta ya petroli, asilimia 4.0 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.

Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la gharama hizo katika Bandari ya Tanga, ambapo zimeongezeka kwa asilimia 3.5 kwa petroli na dizeli na katika Bandari ya Mtwara zimeongezeka kwa asilimia 11.5 kwa mafuta ya petroli, huku kukiwa hakuna mabadiliko kwa mafuta ya dizeli.