Watu watatu wa familia moja wamefariki dunia akiwamo mtumishi wa Wizara ya Maji, Rochi Mkolekuwa (39), baada ya nyumba kuteketea kwa moto Mtaa wa Nyarusrya, Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara.
Mbali na Mkolekuwa aliyekuwa Meneja wa Ubora wa Maji katika Maabara ya Mkoa wa Mara, wengine waliofariki dunia ni mkewe, Mariam Msigwa (34) na mtoto wao, Rochi Shaban (4).
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi tayari umeanza.
Magere amesema walipata taarifa ya tukio hilo saa 10 usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 5, 2026 na walipofika katika nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi walikuta imeteketea na watu hao wakiwa ndani.
"Inaonekana taarifa ilichelewa kutolewa na tulipofika pale tulikuta tayari wamefariki dunia, mwili wa baba ulikutwa sebuleni na miili ya mama na mtoto ilikutwa chumbani, tumeanza uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine," amesema Magere.