Aliyekuwa kiongozi wa Venezuela, Nicolas Maduro, amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza nchini Marekani pamoja na mkewe, Cilia Flores, huku akiendelea kusisitiza yeye bado Rais wa Venezuela.
Maduro na mkewe asubuhi ya jana Jumatatu Januari 5, wamesafirishwa kwa helkopta kutoka eneo walilokuwa kizuizini umbali wa nusu kilomita hadi Manhattan ilipo Mahakama.
Maduro na mkewe wamekana mashtaka yote waliyosomewa na hawakuomba dhamana huku akiendelea kusisitiza yeye bado Rais halali wa Venezuela.
Maduro na mkewe walifikishwa mbele ya Mahakama ya New York baada ya kukamatwa katika operesheni ya kijeshi ya Marekani, hatua ambayo mawakili wake wameitaja kuwa “utekaji nyara wa kijeshi” unaokiuka sheria za kimataifa na misingi ya haki.
Wanakabiliwa na mashtaka mazito yanayohusisha dawa za kulevya na silaha, huku wakichagua kwa sasa kutowasilisha ombi la dhamana.
Akiwa mbele ya Jaji Alvin Hellerstein, Maduro alitamka kwa sauti thabiti:“Mimi sina hatia,” na kuongeza kuwa yeye ni “mtu mwema.”
Alipoulizwa kuthibitisha jina lake, alijitambulisha kama Rais wa Venezuela na kudai alikamatwa nyumbani kwake, tamko lililoibua hali ya tahadhari mahakamani.