Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa Serikali igharamie mazishi ya wote waliopoteza maisha kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara ambapo hadi sasa waliofariki ni Watu 50.
Taarifa imesema Rais Samia ambaye amekuwepo Dubai katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) amefupisha safari hiyo na kurejea nchini ili kushughulikia kwa karibu janga hilo.
Aidha, ameagiza majeruhi ambao wapo Hospitali mbalimbali wapate matibabu kwa gharama za Serikali, pia Wananchi ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda. Idadi za Kaya zilizoathirika ni 1,150, idadi ya Watu walioathirika ni 5,600 na pia ikikadiriwa takriban ekari 750 za mashamba zimeharibiwa.