Kiongozi wa Muungano wa Waasi wa Congo River Alliance unaolijumuisha kundi la wapiganaji wa M23 waliofanikiwa kuuteka Mji wa Goma, Corneille Nangaa amesema lengo lao si kuiteka Goma pekee bali Kinshasa ili kumuondoa madarakani Rais Felix Tshisekedi.
Kauli hiyo inakuja muda mfupi baada ya waasi wa M23 kuushikilia Uwanja wa Ndege wa Goma na maeneo mengine muhimu katika mji huo, huku risasi na mabomu zikiendelea kurindima usiku kucha.
Nangaa ambaye ni swahiba wa Sultani Makenga, kiongozi wa wapiganaji wa M23, amenukuliwa akisema matatizo yanayokabili nchi hiyo yanatokana na uongozi mbovu wa Serikali, hivyo wataiteka Kinshasa ambayo ndiyo makao makuu na kumuondoa Tshisekedi madarakani.
Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo(DRC) imelaani vitendo vya M23, ikitaja kutekwa kwa Goma kama tangazo la vita huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitaka kuondolewa kwa waasi wa M23 na vikosi vingine vya nje kutoka eneo hilo.