Bunge la Ufaransa limepitisha sheria mpya inayowazuia watoto wenye umri chini ya miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii.
Wabunge wa mabunge yote mawili nchini humo walipiga kura kuunga mkono sheria hiyo Jumanne, ambayo pia inapiga marufuku wanafunzi kutumia simu za mkononi wakiwa shuleni.
Hatua hiyo inaifanya Ufaransa kuwa nchi ya kwanza katika Umoja wa Ulaya kupitisha marufuku ya jumla kwa watoto chini ya miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii, huku kukiwa na ongezeko la wasiwasi kuhusu madhara ya maudhui ya kidijitali kwa watoto.
Rais Emmanuel Macron, ambaye amekuwa akiunga mkono sheria hiyo kama moja ya mipango muhimu ya kipindi chake cha pili cha uongozi, amesema kupitishwa kwake ni “hatua kubwa mbele” katika kuwalinda watoto na vijana.
Macron amesema Ufaransa inaongoza barani Ulaya katika jitihada za kulinda watoto mtandaoni. Ameeleza kuwa anataka sheria hiyo ianze kutekelezwa ifikapo Septemba kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo, ingawa mapitio ya kikatiba yanaweza kuchelewesha utekelezaji wake.