Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemteua Meja Jenerali Mykhailo Drapatyi, mwenye umri wa miaka 43, kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ukraine, akichukua nafasi ya Oleksandr Syrskyi aliyekuwa akiongoza jeshi hilo tangu Februari 2024.
Uamuzi huo umefanyika baada ya kuwepo taarifa kuwa Zelensky alikuwa akifikiria kumuondoa Syrskyi kufuatia mabadiliko ya uongozi serikalini na mgogoro uliohusisha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Mykhailo Fedorov.
Kuondolewa kwa Fedorov kulizua maandamano katika miji mbalimbali ya Ukraine, huku waandamanaji wakitaka arejeshwe madarakani, Syrskyi aondolewe na kufanyika mageuzi katika jeshi la nchi hiyo.
Ripoti zinaeleza kuwa Zelensky alizingatia majina kadhaa kabla ya kumteua Drapatyi, huku Fedorov akielezwa kuwa alikuwa ameingia kwenye mvutano na Syrskyi kuhusu uendeshaji wa jeshi.
Kabla ya kuondoka madarakani, Syrskyi alisema jeshi la Ukraine ambalo miaka miwili iliyopita lilikuwa likikabiliana na mashambulizi makubwa, sasa limebadilika na kuanza kufanya operesheni za kukabiliana na maadui.