Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, ametoa wito kwa wanachama, wafuasi na wadau wa mageuzi kuongeza ushiriki wao katika kampeni ya uchangiaji wa fedha kupitia mfumo wa Tone Tone, akisema mchango wa kila mmoja ni muhimu katika kuimarisha shughuli za chama. Amesema hayo kupitia waraka aliouchapisha katika akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Lema ameeleza kuwa kampeni hiyo imeendelea kupata mwitikio mkubwa tangu ilipozinduliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, pamoja na kutangazwa kwa maazimio ya chama na maandalizi ya kikao kijacho cha Baraza Kuu. Ameongeza kuwa viongozi, wanachama na wananchi wameendelea kuhamasishana kuchangia ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Amesema anawashukuru wote waliojitokeza kuhamasisha na kuchangia, akieleza kuwa kila mchango una thamani katika safari ya chama. Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado kuna nafasi ya kuongeza ushiriki kutokana na idadi kubwa ya wafuasi wanaodaiwa kuunga mkono chama hicho.
"CHADEMA ni Chama chenye wafuasi wengi kuliko Chama chochote cha siasa nchini."
Lema amesema wakati wa operesheni ya CHADEMA ni Msingi, chama kilikuwa na kanzidata ya wanachama zaidi ya milioni saba, huku akidai kuwa tathmini za sasa zinaonyesha wapenzi wa demokrasia, haki na mabadiliko wanafikia au hata kuzidi asilimia 65 ya Watanzania wazima.