Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, ameonya wanajeshi na maofisa wa usalama wanaojiunga na maandamano ya upinzani kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria na inaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Katika taarifa iliyotolewa na ikulu ya nchi hiyo jana, Oktoba 12, 2025 Rajoelina amesema serikali haitovumilia jaribio lolote la kuvuruga utawala wa kikatiba, akidai kuwa baadhi ya wanajeshi wanashiriki katika kile alichokiita jaribio la kunyakua madaraka kwa nguvu.
“Tunapaswa kulinda Katiba na kuheshimu taasisi za nchi. Mtu yeyote atakayeshiriki katika uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali,” amesema Rajoelina kupitia televisheni ya taifa hilo.
Taarifa hiyo imekuja kufuatia ripoti za baadhi ya wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha CAPSAT kujiunga na waandamanaji wanaopinga serikali mjini Antananarivo.
Kikosi hicho kiliripotiwa kutangaza kwamba kimemteua Jenerali Demosthene Pikulas kama mkuu wa jeshi jipya, hatua iliyoongeza taharuki ya kisiasa nchini humo.
Hata hivyo, kiongozi wa CAPSAT, Kanali Michael Randrianirina, amesema hawajafanya mapinduzi bali wanataka mabadiliko ya kweli kwa manufaa ya wananchi.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi la Gendarmerie lilisema halitatumia nguvu dhidi ya raia, likisisitiza umuhimu wa mazungumzo.