Baada ya tambo za siku 12, leo watajulikana viongozi wa Chadema kwa nafasi za mwenyekiti na makamu wake katika kanda za Nyasa, Magharibi na Serengeti.
Kanda hizo zinaundwa na mikoa ya Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa.
Uchaguzi katika Kanda ya Nyasa utaamua ama Mchungaji Peter Msigwa atetee nafasi ya uenyekiti baada ya kuiongoza kwa awamu mbili mfululizo kuanzia mwaka 2016 au inyakuliwe na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Mchuano kati ya wawili hao unatarajiwa kuwa mkali, kutokana na umaarufu walionao wawili hao ambao wamewahi kuwa wabunge, Mchungaji Msigwa Iringa Mjini na Sugu (Mbeya Mjini).
Waliingia bungeni 2010 hadi 2020 na pia wote wameshika nyadhifa za ujumbe wa kamati kuu ya chama hicho.