Kenya Yatangaza sikukuu ya Kitaifa kumuenzi Raila Odinga

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

3 hours ago
rickmedia: kenya-yatangaza-sikukuu-kitaifa-kumuenzi-raila-odinga-589-rickmedia

Serikali imetangaza Ijumaa, Oktoba 17, 2025 kuwa sikukuu ya umma kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, aliyefariki dunia jana akipatiwa matibabu nchini India.

Katika tangazo maalumu la gazeti la Serikali Na. 15007 lililochapishwa leo Alhamisi, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, ametangaza tamko hilo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Likizo ya Umma (Sura ya 110).

Mazishi ya kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Nyayo siku ya Ijumaa.

Bendera kote nchini Kenya zimekuwa zikipepea nusu mlingoti tangu Jumatano baada ya habari za kufariki kwa Odinga zilipothibitishwa, huku vitabu vya rambirambi vikifunguliwa katika ofisi za Serikali, balozi na ofisi za chama cha ODM.

Raila Odinga (80), aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya mwaka 2008 hadi 2013 chini ya Serikali ya Muungano kufuatia uchaguzi wa urais wa 2007 uliokumbwa na utata.

Odinga, pia alikuwa mgombea urais mara tano na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).