Mahakama Kuu leo kuamua video ya Tundu Lissu

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

10 hours ago
rickmedia: mahakama-kuu-leo-kuamua-video-tundu-lissu-855-rickmedia

Hatima ya picha mjongeo (video) ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu kupokelewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili mshtakiwa huyo, kujulikana leo.

Uamuzi huo unatarajia kutolewa leo Jumatano Oktoba 22, 2025 na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Ni uamuzi utakaomaliza ubishi ambapo upande mmoja utaibuka na ushindi baada ya mahakama kushawishika na hoja zinazodaiwa kuwa na maudhui (maneno) ya uhaini, katika mkutano wake na waliokuwa watia nia kugombea nafsi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...".

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.