Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini, Mtwara, imewahukumu kifo kwa kunyongwa mapacha wawili, Daniel Stephen Seif (Kurwa) na Daniford Stephen Seif (Doto), wote wakiwa na umri wa miaka 24, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mama yao mzazi, Upendo Methew (42), mkazi wa Kijiji cha Mraushi A, Wilaya ya Masasi.
Tukio hilo lilitokea tarehe 15 Desemba 2024, ambapo mapacha hao walimpiga mama yao kwa kutumia jembe na mwichi, wakidai kuwa alikuwa amewaroga. Walisema walihisi hivyo baada ya mmoja wao kudai kushindwa kushiriki tendo la ndoa, tatizo ambalo walihusisha na ushirikina.
.Baada ya kwenda kwa mganga wa kienyeji, waliambiwa kuwa mama yao ndiye chanzo cha matatizo yao, jambo lililowachochea kurudi nyumbani na kufanya mauaji hayo. Mahakamani, wote walikiri kutenda kosa hilo, na hukumu ya kunyongwa hadi kufa imetolewa dhidi yao.